Header Ads

RAIS PIERE NKURUNZINZA, PAMBANA


Na Happiness Katabazi

MEI 13 mwaka huu, Jenerali wa zamani wa Jeshi la Burundi,Godefroid Niyombare alitangaza kumpindua Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunzinza ' Handsome Boy'.

Lakini muda mfupi baada ya kutangaza mapinduzi hayo, wanajeshi watiifu wa jeshi hilo walipambana na kuakikisha serikali ya Rais Nkurunzinza inaendelea kuwepo madarakani na inasemekana  Mtangazaji huyo wa mapinduzi Niyombare kutokomea kusikojulikana.

Awali ya yote natoa pole kwa wananchi wa Burundi kwa adha wanayoipata kutokana na machafuko ambayo haswa yanachochewa na watu wasiyo na mapenzi mema na Burundi,uchu wa madaraka na wasiotaka kuheshimu utawala wa Sheria na Demokrasia  nchini Burundi. Walaaniwe.

Nina haki ya kujadili matukio ya uvunjifu wa amani na sheria yanayofanywa na baadhi ya Wananchi wa Burundi kwasababu Burundi ni miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo pia sisi Tanzania ni mwanachama.

Hivyo madhara ya vitendo vya uvunjwaji wa sheria , Katiba yanatia doa Juimuiya ya EAC mbele ya uso wa dunia, pia Tanzania inajikuta nayo inapokea wakimbizi kutoka Burundi na nadhara mengine mengi wakati kama wananchi hao  wasingejihusisha na vitendo vya kuvunja sheria madhara hayo yasingetokea.

Nyie wananchi wa Burundi ambao mmejazwa ujinga na wapinzani mkaamua   kuingia mtaani kufanya vurugu kwanini   hamkujiulizi kwanza hao viongozi wa vyama vya upinzani vinavyowashawishi mfanye vurugu,wake na watoto wao mbona hamuungani nao mtaani kufanya vurugu na wote joto la mkondo wa sheria?

Burundi ni  taifa huru ambalo wananchi wake wameamua taifa hilo liongozwe kwa Katiba na Sheria.Na Katiba ndiyo sheria Mama.

Imeripotiwa kuwa Katiba ya Burundi inasema Rais wa Burundi atatakiwa kushika nafasi ya kiti cha urais kwa mihula mihili tu.

Katiba hiyo haitambui kipindi cha mpito.Nkurunzinza amechaguliwa mara moja tu kuwa rais wa Burundu katika uchaguzi mkuu wa kwanza uliofanyika miaka mitano iliyopita na kipindi hicho kinatambulika na Katiba ya nchi hiyo.

Kipindi cha kwanza Nkurunzinza aliingia kushika wadhifa wa rais kwa kuidhinishwa na bunge kwa kipindi cha mpito hivyo ,hakuchaguliwa katika uchaguzi mkuu .

Na Mahakama Kuu ya Burundi hivi karibuni ilitoa tafsiri yake ya kisheria na kusema Nkurunzinza ana haki Kitiba kugombea tena urais na endapo atagombea urais atakuwa hajavunja Katiba ya nchi.

Na hadi sasa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Burundi haujatenguliwa na Mahakama ya Rufaa ya nchi hiyo.Hivyo bado ni uamuzi halali.

Na chama anachokiongoza Nkurunzinza   cha     hivi karibuni kilimruhusu agombee tena urais kwa muhura wa pili kupitia tiketi ya chama chao.

Kwa maana hiyo hoja ya kwamba Nkurunzinza  hatakiwi na wana Burundi wote siyo ya kweli ni hoja mfu maana kama hatawiki chama chake ndio chama tawala na kina wananchi wengi sasa inakuwaje leo hii watu wachache wadai watu wengi hawamuingi mkono.

Na hoja ya kwamba wananchi wa Burundi wamekufa katika machafuko yale kwa sababu eti Nkurunzinza hataki kutoka madarakani,ni hoja isiyo na mashiko kwani marehemu wale walivyokuwa hai wasingeshiriki vitendo vya kuvunja sheria vya kuingia mitaani na kufanya vurugu na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi iliyokuwa ikiwataka watawanyike ,umauti,ulemavu usingewakuta kwani wale wananchi wa Burundi ambao walikataa kuingia mtaani hakuuwawa katika vurugu zile  wala kupata ulemavu.

Kama wana Burundi waliamua taifa lao liongozwe kwa Katiba na Sheria, kwanini sasa hawataki kuheshimu uamuzi wa  Mahakama Kuu ya Burundi ambayo ilitoa uamuzi wake hivi Karibuni na  kusema Nkurunzinza hajavunja Katiba ya Burundi?

Maana Mahakama ndio chombo pekee cha kutoa haki na kutafsiri sheria na Mahakama Kuu ya Burundi ilishatoa tafsiri kuhusu je kipindi cha mpito kinatambulika Katika Katiba ya Burundi ,ikasema hakitambuliki.

Kikubwa zaidi hatusikia wakazi wa Burundi wakilalamika Nkurunzinza ameshindwa kuwaletea maendeleo , kila kukicha tunawasikia wakilalamika  Nkurunzinza amevunja Katiba tena wameanza kulalamika hilo baada ya kusikia chama cha Nkurunzinza kimempitisha tena kugombea nafasi ya urais ?

Halafu kama sio nongwa na choyo ni kitu gani? Kama kweli nyie baadhi ya watu wa Burundi hammtaki Nkurunzinza si msubiri siku ya tarehe ya kupiga kura katika Uchaguzi  Mkuu wa nchi yenu, ndiyo mmpigie kura nyingi za hapa ili ashindwe kutetea nafasi ya kiti cha urais?

Mnafikiri vurugu ni njia sahihi na nzuri?Binafsi mimi ni muumini wa amani na sheria na nilitangaza  maslahi yangu tangu wiki mbili zilizopita kuwa napinga vitendo vya uvunjwaji wa sheria na vinavyofanywa na baadhi ya wananchi wa Burundi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Haya jaribio la kumpindua Rais Nkurunzinza limekwama, nyie wananchi mliokuwa mkijitanguliza mstari wa mbele kuingia mtaani kushiriki vitendo vya uvunjwaji wa sheria vya kushinikiza rais wenu atoke madarakani leo hii sura zenu mtaziweka wapi?

Maana yule Meja Jenerali Niyombare  aliyetimuliwa kazi na Nkurunzinza Februali mwaka huu,ambaye juzi alitangaza mapinduzi ameishatokomea kusikojulikana,  Nkurunzinza ndiyo katuna pale Ikulu mnafikiri nini kitawakuta nyie wote mlioshiriki wazi na kwa  siri kuanzisha machafuko kwa siku kadhaa hapo Burundi ?

Na ninatoa rai kwa baadhi Watanzania tena wengine ni viongozi wa vyama vya upinzani ambao walikuwa wakiunga mkono vitendo vya kihuni hadharani wengine ndani ya Bunge akiwemo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema ambaye jana bungeni bila aibu alizungumza ndani ya bunge kuwa anawapongeza wananchi wa Burundi kwa kumpindua rais wao  hali iliyosababisha Mwenyekiti wa Bunge,Idd Azzan Zungu kumtaka asindelee kuzungumzia mambo hayo.

Vitendo vya uvunjifu wa sheria mitaani  vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya wananchi kuwa Burundi, waache hiyo tabia kwasababu hao wanaojifanya wanawaunga mkono wananchi wa Burundi ni wazandiki na  majuha.

Nasema ni wanafki kwasababu kama wanawapongeza kwa kutenda vitendo vile vya kidharimu kwanini huyo Lema na hao Watanzania wanaowaunga mkono wananchi wale ambao miongoni mwao hivi sasa wapo mikononi mwa vyombo vya dola na wengine wamekimbia kwanini hawaendi Burundi au  kule kule Kigoma kwenda kuwapa misaaada?

Wakazi wa Burundi sijui kwanini hamtaki kujifunza kuwa vita hainaga  macho na kwamba vita hii mnayoitaka miaka ya nyuma iliwaletea madhara makubwa sana?

Burundi ilishakumbwa na vita mkapoteza wapendwa wenu alipoingia Nkurunzinza kwa kipindi chake chote hicho hakuna vita iliyotokea ila sijui mmnaamu vita tena irudi nchink kwenu?

Acheni ujinga huo wakutumiwa ovyo ovyo na baadhi watu wenye uchu wa  madaraka na wenye dhamira mbaya na husuda na Burundi.

Na mtambue sio kila ushauri unaotolewa na wananchi kwa rais wao ,rais halazimiki kuufuta wala kuuzingatia kama ushauri huo auzingatii matakwa ya Katiba na sheria ya taifa husika.

Mfano mzuri ni Ibara ya 37(1) ya  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1979 , inasomeka hivi ;

   "37.-(1) Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba
hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na
shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata
ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale
anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya
jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka
yoyote.".

Kwa minajiri ya Ibara hiyo tunaona kuwa Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa  na mtu yeyote,isipokuwa tu pale  anapotakiwa na Katiba au sheria nyingine yoyote  kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na  mtu au mamlaka yoyote.

Na nina imani viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawatakubali kuona machafuko yanaendelea nchini Burundi,watatumia njia za kidemokrasia na njia nyingine za siri kuakikisha Burundi inakaa sawa na wahuni wanashughulikiwa haraka.

Na leo Rais Nkurunzinza amewasili nchini Burundi akitokea Tanzania na amepokelewa shangwe na nderemo na maelfu ya wafuasi wake.Yupo Ikulu anachapakazi na walioshiriki kufanya mapinduzi baadhi yao wamekamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya dola.

Niitimishe kwa kumpa pole Nkurunzinza kwa niaba ya taifa lake kwa changamoto inazopitia ninaimani Mungu atalivusha salama taifa la Burundi na mtendeneane haki kwa mujibu wa sheria na sio misukumo ya uchu wa madaraka wa kutaka madaraka kwa njia haramu ambazo wana Afrika  Mashariki hatutaki wananchi wenzetu kutoka katika nchi zinazounda Jumuiya ya EAC watumie njia za mapinduzi kuingia madarakani.

Jumuiya ya  EAC bado ni changa ukilinganisha na Jumuiya za  mataifa mengine makubwa duniani,hivyo bado tunaitaji kuwa na Jumuiya imara ambayo moja ya nchi yake hatutairuhusu kirahisi kiingie kwenye vita kwani njia za kidiplomasia za kusuluhisha migogoro zipo na Wanadiplomasia wazuri tu wapo katika EAC na historia inaonyesha Wanadiplomasia hao wameishawahi kusuluhisha  migogoro katika baadhi ya nchi ikiwemo  mgogoro nchini Kenya inayotokea nyakati za uchaguzi ambao ni  Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na wengine.

Mungu ibariki Tanzania

Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com
Facebook: Happy Katabazi
0716 774494

Mei 15 mwaka 2015.

No comments:

Powered by Blogger.