Header Ads

NAENDELEA KUKULIA WAKILI STANSLAUS BONIFACE ' JEMBE', 2015




Na Happiness Katabazi

Leo  Mei 27 mwaka  2015, mpendwa wetu  aliyekuwa Wakili Kiongozi wa Serikali mwenye  cheo cha Mkurugenzi  Msaidizi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface Makulilo ‘Jembe’ anatimiza miaka mitatu tangu afariki ghafla  tarehe kama ya leo Mei 27 mwaka 2012 katika  Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.

Kila mwaka tarehe kama ya leo nimekuwa nikiandika makala ya kumbukizi ya kifo cha marehemu Boniface kwasababu wakili huyu Mwandamizi nilikuwa nikiheshimu na nitaendelea kuheshimu na kuthamini mchango wake kwa serikali kupitia taaluma yake ya sheria k hasa katika eneo la uendeshaji wa mashitaka kwa niaba ya Jamhuri.

Nilifahamiana na Boniface katika mahakama za Dar es Salaam tangu mwaka 2008.

Kilichotuunganisha mimi na Kaka Boniface ni kazi za ujenzi wa taifa tulizokuwa tukizifanya mahakamani katika mahakama hizo.

Yeye alikuwa ni wakili wa Serikali na mimi nilikuwa Mwandishi wa habari za mahakamani wa gazeti la Tanzania Daima.

Hivyo tulifanyakazi pamoja na nilipoanza safari yangu ya kuanza kusoma fani ya sheria mwaka 2009 hadi sasa Boniface naye kama walivyo baadhi ya majaji,mahakimu,wanasheria mbalimbali waliokuwa wakinipa moyo nisome fani ya sheria.

Boniface alikuwa akishiriki wakati mwingine kunifundisha baadhi ya topic na alikuwa akinipa sheria mbalimbali ambazo hadi sasa zinanisaidia katika masomo yangu ya kozi ya sheria.

Kwa wale tuliopata fursa ya kuwa karibu na Boniface kikazi na kijamii ama kwa hakika si majaji, mahakimu,wapelelezi wake na walalamikaji katika kesi za jinai,waandishi wa habari za mahakamani hakika wengi wetu tunakiri wazi wazi serikali ilipoteza Mwendesha mashitaka mahiri ambaye uenda alipokuwa hai watawala waliokuwa wameshika nyadhifa za juu serikalini walikuwa hawafahamu vizuri kipaji alichokuwa nacho Boniface cha kutumia taaluma yake ipasavyo kuipigania serikali katika kesi zake kwa ufundi wa kisheria wa hali ga juu.

Boniface nakumbuka mbwembwe zako za kiuwakili wa serikali ulizokuwa ukionyesha mahakamani na wakati ukijitambulisha mbele ya hakimu au jaji anayesikiliza kesi uliyokuwa ukiiendesha ulikuwa ukipenda kutumia neno hili ' Ikupendeze Mheshimiwa jaji,hakimu'  kisha unaweka mkono mfukoni unatoa,unendelea 'kusilisha hoja  wewe ulikuwa ukipenda kusema (una mwaga vitu) huku 'ukiswing ' kwenye 'bar'.

Yaani ukionyesha mikogo ya wanasheria  katika eneo wanalokaa mawakili kuendeshea kesi wakati kesi ikiendelea.

Boniface alikuwa ni tishio kwa baadhi ya mawakili ambao wanakuwa hawajipanga vyema kuwatetea wateja wao na alikuwa tishio kwa washitakiwa wa kesi alizokuwa akiziendesha.

Ndio maana Boniface alipo fariki kuna wengine tulilia sana kwakujua tumepoteza wakili mahiri wa serikali.

Lakini wanaopenda uhalifu na washitakiwa baadhi ambao Boniface alikuwa ni mwiba kwako walifurahia sana kwakusema kizingiti kimeondoka.

Lakini kikubwa zaidi ulipokuwa mahakamani ukiona shahidi anataka kukuchezea akili ulikuwa ukiomba kutoka nje unakwenda kwenye kordo za mahakama na kuvuta 'Fegi'  zako kisha unarudi mahakamani kutwanga shahidi kwa hoja za kisheria.

Nilivutiwa sana na umahiri wa uendeshaji wa mashitaka uliokuwa ukifanywa na kaka Boniface.

Boniface leo ukiwa unatimiza miaka mitatu tangu ulipofariki dunia ,kikubwa kilichojiri katika tasnia ya eneo la sheria katika serikali ni aliyekuwa Mkuu wako wa Kazi Mkurugenzi wa Mashitaka  DPP- Dk.Eliezer Feleshi ,Agosti 13 mwaka 2014,  Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Jaji wa  Mahakama Kuu na ofisi yake ni Kanda ya Dar es Salaam, yupo anaendelea kupiga mzigo.

Pia kijana wako Biswalo Mganga ambaye mlikuwa mkifanyaka nae kazi katika ofisi ya DPP, Oktoba 6 mwaka 2014 alipandishwa cheo baada ya  Rais Kikwete kumteua kuwa  Mkurugenzi mpya wa  mashitaka  nchini (DPP) kurithi nafasi iliyoachwa wazi ni Dk.Feleshi.

Pia Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju ,Januari 2 mwaka 2015  ,aliteuliwa na rais kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema, Disemba 16 mwaka huu,  kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichoeleza kuwa ushauri wake alioutoa katika Akaunti ya Tegeta  Escrow umeeleweka vibaya.

Naye AG- Masaju anafanyakazi yake vizuri ila ndiyo hivyo tena hatutamuona tena mahakamani akiendesha mashauri mbalimbali kwa niaba ya serikali kwa sababu amepandishwa cheo.

Mganga anaendelea na kazi yake hiyo vizuri tu na bado hajaanza kufanya ufisadi na nilimuaidi katika makala niliyomuandikia wakatj alipoteuliwa kushika wadhifa huo kwamba nikibaini ameanza kuwa fisadi wa kikweli kweli basi nitamuanika kupitia makala zangu bila huruma.

Kwa upande wangu mimi Happiness Katabazi, Agosti Mosi mwaka 2014 niliachakazi rasmi katika gazeti la Tanzania Daima  na kwenda kuwa Ofisa Habari wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo,Mikocheni Dar es Salaam na wakati huo naendelea kusoma kozi yangu ya Sheria kama ulivyokuwa ukiniasa.

Kwa sabababu hivi sasa sio Mwandishi tena wa habari za mahakamani kama zamani na napo majariliwa Agosti mwaka huu,nitakuwa nikienda mahakamani kufanya mazoezi ya kwa vitendo(field) kama mwanafunzi wa Shahada ya Sheria na siyo tena kwenda mahamani kwa kofia ya Uandishi wa habari. kwenda kuripoti kesi mbalimbali.

Katika Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, kesi zenye mvuto zilizofunguliwa kuanzia mwaka jana hadi sasa ni kesi ya Ugaidi inayomkabili
Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid  Ahmed (44).

Kesi hiyo ambayo  haina dhamana hivyo wapo gerezani na kila siku baadhi ya washitakiwa toka  Zanzibar hawaishi kutoa malalamiko yao katika Mahakama ya Kisutu kwamba watagoma kula, mara wasipoachiriwa huru watafanya kitendo ambacho kitashangaza umma, mara walivyokuwa gerezanki kule Zanzibar walilawitiwa sana gerezani hivyo wamearibika sana sehemu za siri za mihili yao na mbaya zaidi jeshi la Magereza haliwapatibabu kwani wanazidi kuaribika sehemu zao za siri  na wakiletwa mahakamani wanaletwa chini ya ulinzi mkali sana wa askari Magereza.

Kesi nyingine iliyofunguliwa na Jamhuri ni kesi dhidi ya wahitimu wa mafunzo ya JKT ambao mwaka huu ,wahitimu hao walizusha taaluki katika jamii wakishitishia wataandamana kwasababu hawajapewa ajira hali iliyosabishwa kukamatwa na kushitakiwa na DPP- Mganga akawasilisha ombi chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 la kufunga dhamana kwa wahitimu ambao hadi sasa wapo gerezani na wamekuwa na nidhamu maana walikosa nidhamu.

Kesi nyingine inayovuta hisia za watu wengi ni kesi ya uchochezi inayomkabili Sheikh Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro ambayo inaendelea licha Ponda yupo gerezani kwa sababu DPP alimfungia dhamana.

Ile kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh.bilioni 11 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha,Basil Mramba na wenzake ambayo ulianza kuiendesha imefikia hatua washitakiwa wameishamaliza kujitetea.

Kuhusu kesi za EPA ,Kada wa CCM, Shaban Maranda amemaliza kifungo chake katika kesi zilizokuwa zikimkabili,ila Farijala Hussein alimaliza kifungo chake na akarudi uraiani huku akiendelea na kesi zake lakini mwaka huu, amerudishwa gerezani baada ya kupatikana na hatia.

Kuhusu zile jumla ya kesi 11 za wizi katika akaunti za EPA katika Benki Kuu, ambazo wewe (Boniface)na mawakili wenzako mlikuwa mkiziendesha na hadi unakutwa na mauti uliweza kufanikiwa kushuhudia kesi moja ya EPA ya wizi wa sh.bilioni 1.3 iliyokuwa ikimkabili Rajabu Maranda na Farijala Hussein wakihukumiwa kwenda jela miaka mitano, na ulivyofariki pia tayari kuna hukumu za kesi mbili za EPA ambazo zinamhusisha Maranda ,Farijala na maofisa wa BOT watatu zilitolewa hukumu. Hivyo kesi nyingine za EPA zilizosalia bado haizajatolewa hukumu .

Ila zile kesi nne za EPA zinazomkabili mfanyabiashara maarufu Jeetu Patel  zilizofunguliwa Novemba 2008 bado hata shahidi mmoja wa upande wa jamhuri hawajaanza kupanda kizimbani kuanza kutosha ushahidi wake.

Hizo ni simulizi chache za baadhi ya kesi zilizovuta hisia katika jamii na sisi waandishi wa habari kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja ambacho wewe haupo nasi duniani.

Ila napenda nikuakikishie tu kuwa mawakili wa serikali bado wanatupatia ushirikiano wa kutosha sisi waandishi wa habari za mahakamani kama zamani.

Unakumbukwa na waandishi wa habari za mahakamani wenzangu Furaha Omary, Magai James, Tausi Ally, Faustine Kapama, Kulwa Mzee,Grace Gurisha, Frola Mwakasala ,Karama ,Hellen Mwango.

Lakini bado unakumbukwa na mawakili na Jaji Dk.Eliezer Feleshi, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Duwani Nyanda , DPP- Biswalo Mganga, Malangwe Mchungahela, Tumaini Kweka ,Sedekia Emphere,Fredrick Manyanda,Oswald Tibabyekomya, Lasdslaus Komanya, Tumaini Kweka, Ponsian Lukosi,Ben Lincoln,Arafa Msafiri, Timon Vitalis,Michael Lwena ,Bernad Kongora na wengine wengi.

Ambao kwa kadri ya uwezo wao wanafanya vizuri katika majukumu yao ya uendeshaji wa mashitaka, na wengi niliozungumza nao wanakushukuru kwa mchango wako wa kitaaluma kwani hukuwa mchoyo wa kuwafundisha kazi pale walipoitaji msaada huo.

Miongoni mwa kesi kubwa ambazo mimi binafsi nilimshuhudia  Marehemu Boniface  akiziendesha kwa zaidi ya miaka mitano katika mahakama mbalimbali hapa nchini sasa ni kesi ya wizi wa shilingi bilioni 1.8 katika EPA, iliyokuwa ikimkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambapo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 23 mwaka juzi, iliwahukumu kwenda jela miaka mitano, kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC, Jerry Murro na wenzake ambapo Murro alishinda kesi hiyo mwaka juzi.

Kesi  ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabishara Jayankumar Patel “Jeetu Patel’ na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DPP na Reginal Mengi iliyokuwa akitaka afutiwe kesi zake nne za EPA zilizopo katika mahakama ya Kisutu kwasababu Mengi alimuhukumu kabla ya hajahukumiwa na mahakama kwa sababu alimuita ni Fisadi Papa, ambapo Boniface alimwakilisha AG na DPP na aliibuka mshindi katika kesi hiyo.

 Kesi nyingine kubwa ambayo marehemu alikuwa akiziendesha ambazo bado hadi umauti unamkuta hazijatolewa hukumu ni ile ya mauji ya Ubungo Mataa ambayo Disemba 19 mwaka 2014,Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Jaji Projestus Rugazia  alitoa hukumu ya kesi hiyo ambayo pia Boniface aliendesha na miongoni mwa Mashahidi wa upande wa Jamhuri ni Kamishna Msaidizi Duwani Nyanda .

Jaji Rugazi akitoa hukumu yake katika kesi hiyo ambayo ilikuwa na vitimbi vya kila aina alisema mahakama yake  imewahukumu kunyongwa hadi kufa  washtakiwa sita  katika kesi ya mauaji ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa mkoani Morogoro na mfanyakazi wa Benki ya NMB.

Mauaji hayo ambayo yalipata umaarufu na kupewa jina la mauaji ya 'Ubungo Mataa 'yalifanyika Aprili 20,2006  katikati ya Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam.

Jaji Projest Rugazia aliwataja  washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kuwa ni Mashaka Pastory, John Mndasha, Martine Mndasha, Haji Kiweru,  Wycliff Imbora na Rashidi Abdikadir.

Jaji Rugazia alisema aliwatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa,  kufuatia ushahidi ulitolewa na mashahidi 29 wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 78 vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa utetezi.

“Maungamo ya washtakiwa, ushahidi wa kitaalam na utambuzi wa washtakiwa kutambuliwa eneo la tukio inaonesha wazi walikuwa na nia ya kujaribu kupora takribani Sh 150 milioni mali ya benki ya NMB zilizokuwa zikisafirishwa kutoka  Dar es Salaam kwenda  Morogoro tawi la Wami.” Alisema Jaji Rugazia.

Alisema siku hiyo ya huzuni  ya Aprili 20,2006  majambazi hao walilivamia gari  hilo kwa lengo la kupora lakini  bila ya kuwa na huruma yoyote walilimiminia risasi na kuwaua  D 6866 Konstebo Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi.

Walifanya tukio hilo nyakati za saa 6:30 mchana, eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Jaji Rugazia aliwaachia huru washtakiwa Rashid Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,

Hamisi Daud, MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162 Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi hiyo.
Kwa upande wa washtakiwa, Jackson Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo na Mussa Mustafa aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu.

Hadi wanaachiwa huru siku hiyo ya Disemba 19 2014, washtakiwa hao walikuwa wamekwisha kaa  rumande kwa muda wa zaidi ya miaka nane.

Kesi nyingine aliyokuwa akiiendesha Boniface ni rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomwona mfanyabiashara Naeem Gile ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Laurence Kaduri ambaye alikuwa akikabiliwa na makosa ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LCC, kuwa hana kesi ya kujibu, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Kisutu iliyomuona Jerry Murro hana hatia na kesi ya matumizi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 inayomkabili waliokuwa mawaziri wa Fedha na Nishati, Basil Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja ambapo kesi hii hivi sasa imefikia hatua ya Mramba kuendelea kujitetea

Boniface alizaliwa Februali 21 mwaka 1968 ameacha mke na watoto watatu, aliitimu shahada ya kwanza ya Sheria mwaka 1995 na shahada ya pili ya sheria alimaliza mwaka 2008 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Julai Mosi mwaka 1995 aliajiriwa rasmi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kama Wakili wa Serikali, ilipofika Oktoba Mosi mwaka 2006 alipandishwa cheo na kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi.

Oktoba Mosi mwaka 2007 alipandishwa cheo tena na kuwa Wakili Kiongozi wa Serikali.

Nyadhifa ambazo Boniface aliwahi kuzishika enzi za uhai wake ni kati ya mwaka 2003-2007 alikuwa ni Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Mbeya.

Kati ya Mei 2007 na Oktoba 2010 alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi Kanda ya Mwanza.

Novemba 2009 hadi Novemba 2010 alikuwa Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali mkoani Dar es Salaam. Kutokana na utendaji kazi wake mzuri ilipofika Disemba 2010 hadi mauti yanamkuta aliteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha uendesha mashitaka na pia awaka Msimamizi wa uendeshaji kesi zenye maslahi kwa umma. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake liimidiwe.

Leo umetimiza miaka mitatu  tangu Boniface ufariki dunia Mei 27  na Mei 29 mwaka 2012 ulizikwa katika Makaburi ya Kinondoni Dar es Salaam mwaka 2012. Naendelea kukulia Wakili Stanslaus Boniface ' Jembe'.

Chanzo:Blogg: www.katabazihappy.blogspot.com
0716 774494
Mei 27 mwaka 2015

No comments:

Powered by Blogger.