~ Kwa maoni yoyote kuhusu kazi zangu, niandikie katabazihappy@yahoo.com, au nipigie simu namba +255 755 312859. Asante kwa kunitembelea!~
Tuesday, June 30, 2009
DECI WAKWAMA TENA KISUTU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imekataa kurudia kutoa uamuzi wa dhamana wa kesi ya vigogo wa Taasisi ya Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) kwa sababu tayari Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Addy Lyamula alishaitolea uamuzi.


Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi, Mteite, muda mfupi tu baada ya mawakili wa utetezi kuwasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo iziondoe sababu zilizosababisha DPP-Eliezer Feleshi, Juni 17 mwaka huu, kutoa hati ya kuzuia dhamana ya washitakiwa, kwa madai sababu hizo hivi sasa hazipo tena.

Kitululu alidai sababu hizo hazipo tena kwani awali shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza, na upande wa mashitaka ukawa umejengewa uwoga, hivyo DPP akafikia uamuzi wa kutoa hati hiyo ya kuzuia dhamana, ili kulinda usalama wa washitakiwa na maslahi ya Jamhuri.

“Siku hiyo kulikuwa na Maaskari wengi hapa Mahakamani hata wale wa kutuliza ghasia, ni ni dhahiri leo pia hawapo (jana), jambo ambalo limedhihirisha kuwa upande wa serikali umeridhika na hakuna wasiwasi wa kiusalama dhidi ya wateja wetu;

“Na kwa misingi hii tunaomba upande wa mashitaka uiondoe hati hiyo ya DPP ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa ili wateja wetu waweze kupata dhamana kwani shitaka linalowakabili linadhamiwa” alisema Kitululu.

Akipangua hoja hizo wakili wa serikali, Biswalo Mganga, alianza kwa kusema yeye ana majibu mafupi kwamba upelelezi huo bado haujakamilika.

Mganga alidai kesi hiyo ilipokuja kwa mara ya pili Juni 17, mwaka huu, pamoja na mambo mengine yote, Hakimu Mkazi Lyamuya alitoa uamuzi kuhusu dhamana ya washitakiwa, uamuzi ambao alidai umemfunga mikono hata Hakimu Mteite na mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kutengua hati ya DPP.

Mganga akipangua hoja hizo huku akionyesha kujiamini, alidai hati hiyo ni ya DPP na bado DPP hajawasilisha taarifa ya kuiondoa.

Kuhusu hoja ya sababu za kiusalama baina ya washitakiwa na jamhuri , alidai sababu hizo zilitolewa na DPP na wala siyo Kitululu hivyo ni vema DPP mwenyewe akatoa taarifa ya kuiondoa hati hiyo.

Kuhusu hoja kwamba FFU na wanausalama kutokuwepo kwa wingi jana mahakamani hapo, alisema

“Hivi wale nyuma ni Mgambo?si maofisa wa polisi na wakili huyo asitake kuvifundisha kazi vyombo vya ulinzi na usalama kazi kwani vyenyewe vinajua ni jinsi gani vinavyofanyakazi” alidai Mganga na kusababisha watu kuangua kicheko.

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mkazi Mteite, alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa tu na kwamba amesikiliza hoja za pande zote mbili na kueleza kuwa kuhusu hoja za upande wa utetezi kutaka wateja wake wapatiwe dhamana, hawezi kutolea maamuzi ombi hilo kwa mara ya pili kwani Hakimu Lyamuya alishalitolea uamuzi .

Lakini Mteite aliutaka upande wa mashitaka uangalie kama zile sababu zilizoainishwa kwenye hati ya DPP kama hivi sasa hazina nguvu tena, basi waziondee ili washitakiwa waweze kupatiwa dhamana na akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai 10 mwaka huu.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Jackson Mtares Dominic Kisendi, Timotheo ole Loitgimnye, Samwel Mtares, Arbogast Kipilimba na Samwel Mtalis ambao wote wanaendelea kusota rumande.

Juni 12 mwaka huu, Wakili Kiongozi wa Serikali Justus Mlokozi alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na mashitaka mawili, shitaka la kwanza ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1)(3)cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu , na shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha Na.5 ya 2006.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Julai mosi, 2009
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 5:55 PM | Permalink | Maoni 0
SERIKALI YAWEWESEKA MGOMBEA BINAFSI
Na Happiness Katabazi

KWA mara ya pili, serikali imekata rufaa dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Democrat (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, katika Mahakama ya Rufani nchini, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ulioruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu.


Kwa mujibu wa rufaa hiyo namba 45 ya mwaka huu, inaonyesha serikali iliwasilisha rufaa hiyo, Ijumaa iliyopita mahakamani hapo ikipinga hukumu ya iliyotolewa na waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu, ambao ni Jaji Mstaafu Amir Manento, Salum Massati, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Thomas Mihayo (Mstaafu), ambao walikubaliana na ombi na Mtikila na kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi nchini.

Katika rufaa hiyo, serikali imetoa sababu sita za kukata rufaa hiyo zikiwemo; Mahakama Kuu ilikosea kujipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ilikosea kutengua vifungu vya Katiba ya nchi, na kukosea kisheria kwa kupunguza matakwa ya lazima ya Ibara 30(5) na 13(2) ya Katiba ya nchi.

Sababu nyingine ni kujipachika mamlaka ya kibunge ya kutunga sheria, kukosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na pia ilikosea kuitolea maamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana.

Mara ya kwanza, serikali ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika Mahakama hiyo ya Rufaa mwaka 2007, ambapo ilidai mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1)(c), 39(1)(c) (b) na 69(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama ya Rufaa baada ya kukubalina na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza kwamba, rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.

Awali katika hukumu ya Mahakama Kuu uliotolewa Mei 2006, ililiruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mahakama Kuu ilibainisha kuwa Katiba inatamka wazi kuwa, kila mwananchi ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na haiweki masharti kuwa hilo lifanyike kwa mtu kujiunga na chama fulani.

Mwaka 1993, Mtikila alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, lakini licha ya uamuzi huo wa mahakama, Bunge lilishindwa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi hivyo alifungua kesi hiyo ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kushinda tena.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Julai mosi, 2009
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 5:39 PM | Permalink | Maoni 0
TUWE MAKINI MBINU CHAFU ZA UCHAGUZI MKUU ZIMEISHAANZA
Na Happiness Katabazi

WATANZANIA wenzangu kaeni mkao wa kula, msimu wa uchaguzi (mavuno) umewadia, hilo ndilo ambalo naweza kulisema kuhusu pilikapilika na hekaheka za maandalizi ya wagombea uenyekiti wa serikali za mitaa na vijiji, udiwani, ubunge na urais.

Mara nyingi, wananchi tumekuwa hatupo makini katika kuchagua viongozi kwa kuwa tunauona uchaguzi kama sehemu ya kuvuna fedha kutoka kwa wagombea.

Lakini tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameshabainisha kuwa, serikali imeandaa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ili kuondoa vifungu vinavyohalalisha takrima (rushwa).

Kauli hiyo ya Pinda inaonekana kukosa mashiko wa wagiga kura na wagombea kwa kuwa kila mmoja anajiona ana haki ya kutoa au kupokea takrima.

Tayari huku mitaani hivi sasa zimeshaanza pilikapilika kabambe kwa wagombea watarajiwa kutoa hongo kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufadhili timu za mipira ya miguu, kuanzisha mashindano na kutoa vikombe vinavyopachikwa majina yao, kutoa misaada kwa vikundi vya waathirika vya ukimwi na SACCOS.

Walengwa wakuu wa takrima hizo ni vijana na wanawake kwa kuwa wao ndio wanaonekana kuwa ni rahisi kurubuniwa na kupokea rushwa.

Si jambo la kushangaza hivi sasa wapanbe wa wagombea hao kuanza kubisha hodi misikitini na makanisani kwa lengo la kutoa misaada mbalimbali pamoja na kujenga nyumba hizo za ibada.

Katika kipindi hiki, wagombea watakuwa wacha-mungu zaidi pamoja na kutembelea maeneo mbalimbali ilimradi wawe karibu na wananchi kwa lengo la kuwapumbaza.

Tunatakiwa tujiulize maswali magumu, fedha hizi wanazozigawa wapambe wa wagombea hao watarajiwa wamezipata wapi? Au kuna EPA mpya ambayo hatujaigundua?

Sina shaka kuwa kuna uhusiano wa karibu wa wingi huo wa fedha hizo zinazoanza kutapanywa na kupungua kwa mapato ya serikali yanayokusanywa na TRA.

Sababu zinazotolewa za kuyumba kwa uchumi kuwa ndiyo kiini cha kupungua kwa mapato ya nchi, yaweza kuwa kiini macho. Wakati ukifika tutabaini hilo.

Lakini pia tutupie macho yetu kwenye eneo ambalo limekuwa likilindwa na serikali kwa usiri mkubwa, yaani mikataba ya uwekezaji na tenda za manunuzi ya umma.

Naamini kwamba ufisadi katika maeneo haya haujaguswa kana kwamba haupo, lakini najua mabilioni ya serikali hulipwa kila mara kwa mikataba isiyo na tija kwa taifa, kuna kandarasi na tenda za manunuzi ya umma zinazosukwa kwa madhumuni ya kuiba mabilioni ya fedha za umma.

Miradi mingi inayofanywa hivi sasa na serikali inakuwa na mazingira ya watu kunufaika zaidi (ufisadi), ujenzi wa barabara, utengenezaji wa vitambulisho vya uraia vimetengewa fedha nyingi, lakini ukija kuangalia gharama halisi unaweza kuzimia.

Wakati mwingine ufisadi huu wa kuibia umma ufanyika mchana kweupe, kwani barabara zinazojengwa huharibika kabla ya kipindi kifupi tu baada ya kuanza kutumika.

Kwa nini jamii isiamini kwamba baadhi ya wanasiasa na watendaji serikalini wameshajichotea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani?

Kuna tatizo gani katika kufuatilia mambo hayo? Mbona tuna vyombo vya usalama vingi? Idara ya Usalama wa Taifa inayoongozwa na kiongozi shupavu, Rashid Othman ipo, TAKUKURU chini ya Dk. Edward Hosea ipo. Je, hawajatambua maovu hayo?

Nina uhakika itakapofika mwaka 2011 zitaibuliwa kashfa za watu waliojichotea fedha za wananchi na kuzitumia katika uchaguzi.

Binafsi sijaona tija yoyote ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, maarufu kama ‘mabilioni ya JK’, kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali. Pia nina shaka hata hizo sh trilioni 1.5 zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi, zinaweza ziende ninakotarajia.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, walishawahi kuliambia taifa kuwa nchi yetu haitaathirika na mtikisiko wa uchumi, lakini sasa ni tofauti je, nani aaminike?

Najua hakuna atakayeweza kuzuia fedha zilizotengwa na Rais Kikwete kwa ajili ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi zisitumike vibaya, wadadisi wa mambo wanaona fedha hizo zimewekwa kwa ajili ya uchaguzi, hasa kwa chama tawala ili waseme wameshinda kwa kishindo.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Julai 28,2009
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 3:09 PM | Permalink | Maoni 0
Friday, June 26, 2009
WAZEE WA BARAZA WAMTETEA ZOMBE
*Waiambia korti hana hatia
*Wengine ushahidi wawabana
*Sasa yasubiriwa hukumu

Na Happiness Katabazi

WAZEE wa Baraza katika kesi ya mauaji ya wafanyabishara watatu na dereva taksi mmoja inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake nane, wameiomba Mahakama Kuu imwachie huru Zombe kwa kuwa hana hatia.


Wazee hao wa baraza, Magreth Mossi na Nicolus Kimolo, walitoa kauli hizo jana alipokuwa wakitoa maoni yao kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na pande zote mbili.

Mbali na kuomba Zombe kuachiwa huru wazee hao pia wameimba mahakama kumwachia huru mshitakiwa mwinigine katika kesi hiyo, Festus Gwasabi (mshitakiwa wa 13) kwa maelezo kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa hao haukuweza kudhibitisha kuhusika na mauaji hayo.

Kabla ya wazee hao kutoa maoni hayo jana, Jaji wa Mahakam ya Rufani, Salum Massati, anayesikiliza kesi hiyo juzi aliwatahadharisha kutoa maoni yao kwa kutozingatia yaliyoandikwa katika vyombo vya habari kwani yameandikwa mengi kuhusiana na kesi hiyo.

Hata hivyo, katika kutoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji anaweza kuzingatia au kutozingatia maoni ya wazee hao.

Mzee wa baraza aliyeanza kutoa maoni yake ni Kimolo ambaye alieleza kuwa kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka, hakuna shahidi aliyedhibitisha kwamba Zombe alishiriki katika mauaji hayo na pia hakuna shahidi aliyethibitisha alimuona Zombe kwenye eneo la tukio.

Mzee wa Baraza Kimolo ndiye aliyaanza kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusu mshitakiwa wa kwanza(Zombe), alikumbusha upande wa mashitaka ulileta mashahidi 37 na hakuna udhibitisho kwamba mshitakiwa huyo alishiriki katika mauji hao na kwamba hakuna shahidi hata mmoja aliyeweza kusema wala kuthibitisha kwamba walimuona Zombe kwenye eneo la tukio.

Kimolo alidai kuhusu hoja iliyotolewa na upande wa mashitaka kwamba Zombe alikwenda kituo cha Polisi Urafiki, yeye ameona mshitakiwa huyo alikwenda kutatua utata wa fedha na alitoa amri kwamba kielelezo hicho kitimie na kuongeza hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Zombe aende kituoni hapo.

Kuhusu hoja ya mashitaka kwamba Zombe aliwapa mkono wa pongezi askari kuwa alikuwa anajua kilichokuwa kinaendelea kwani asingeweza kutoa pongezi kwa baadhi ya askari; alidai kwa maoni yake Zombe alikuwa hajui chochote kilichokuwa kinaendelea.

Alikumbusha kuwa mahakama hiyo ilielezwa na mshitakiwa wa 12,Rajabu Bakari jinsi walivyofundishwa na Zombe kujibu maswali kwenye Tume ya ACP-Mgawe na Jaji Mussa Kipenka, pia aliendelea kueleza kuwa mshitakiwa wa kwanza aliwapa vikaratasi vya kujitetea lakini Rajabu wakati akijitetea alidai hata hayo aliyofundishwa kujitetea hayakumsaidia na hata alipotakiwa na mahakama atoe hivyo vikaratasi alishindwa kuwasilisha mahakamani vikaratasi hivyo.

“Maoni yangu katika hilo hilo , kushindwa kwa Rajabu kuwasilisha vikaratasi hivyo hayana ukweli” alidai Kimolo huku akionyesha kujiamini.

Akichambua ushahidi wa shahidi wa 36 wa upande wa mashitaka,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Sidney Mkumbi ambaye ndiye alikuwa Mpelelezi Mkuu wa kesi hiyo, alikiri mbele ya mahakama hiyo kuwa Zombe akuandika maeleszo ,pia alieleza mahakama kuwa mshitakiwa wa kwanza ameunganishwa tu kwenye kesi hiyo kutokana na maelezo ya nyongeza yaliyotoka kwa washitakiwa wenzake.

“Baada ya washitakiwa wote kupewa haki yao ya msingi ya kujitetea katika mahakama hii tukufu,hatukuweza kusikia hayo maelezo ya nyongeza yaliyofanya Zombe aunganishwe kwenye kesi hii.

“Jaji ili mahakama yako iweze kumtia hatiani kwa kosa kubwa kama hili mauji nilazima upande wa mashitaka uthibitishe bila kuacha shaka yoyote kesi yake.Hivyo basi upande wa mashitaka katika kesi hii umeshindwa kuthibitisha mashitaka manne ya mauji kwa Zombe kwa sababu zifuatazo:alidai Kimolo.

Sababu ya kwanza alieleza kuwa hakuna shahidi hata mmoja katika mashahidi 37 aliyedai Zombe kuwa alihusika.Pili, Tume zote zilizoundwa,hazikupendekeza mshitakiwa huyo wa kwanza ashitakiwa.Tatu, mpelelezi Mkuu wa kesi hiyo, SACP- Mkumbi naye alithibitisha kwamba Zombe aliunganishwa katika kesi hiyo kwa maelezo ya nyongezo yaliyotolewa na washitakiwa wenzake.

“Kwa maoni na mapendekezo yangu, naiomba mahakama hii imuone Zombe hana hatia kwa makosa ya mauji aliyoshitakiwa nayo” alidai Kimolo.

Kwa upande wake Magreth Mossi, akitoa maoni na mapendekezo yake kuhusu Zombe,alieleza kuwa ni ukweli usiopingika mashahidi wote wa upande wa mashitaka ,hakuna shahidi aliyeweza kuthibitisha shitaka hili kuhusu mshitakiwa huyo.

“Jaji, kuanzia kukamatwa kwa marehemu na hadi walipofikwa na umauti wao hata shahidi mmoja hakuweza kumnyoshea kidole Zombe kuwa alikuwepo eneo la tukio.Mahakama hii ilipokea ushahidi wa jinsi mshitakiwa huyo alivyokuwa akitoa taarifa alizokuwa amezipata kutoka kwa askari wake waliokuwa eneo la tukio” alidai Mossi.

Kuhusu hoja ya Zombe aliwapongeza askari kwamba ilionyesha alikuwa akifahamu tukio hilo, alidai ukweli usiopingika kiongozi yoyote anapoona askari wake wamefanyakazi ya ushupavu sio vibaya kutoa mkono wa pongezi,kwani alipata taarifa askari wake walikamata majambazi na silaha waliopora roli la kampuni ya Bidco.

“Naona hicho ndicho kilimfanya Zombe kutoa mkono wa pongezi na tume zote mbili zilioundwa , hazikumuona mshitakiwa huyo ana kesi ya mauji hivyo naungana na mzee wa baraza mwenzangu, kuiomba mahakama hii tukufu umuone mshitakiwa wa kwanza hana hatia” alidai Mosi, na kusababisha Zombe awe anajifuta machozi mara kwa mara kizimbani.

Kuhusu mshitakiwa 13, Festus Gwasabi, wazee hao wote kwa pamoja waliomba mahakama imuone hana hatia kwani ushahidi umeonyesha alishiriki katika upekuzi wa kwa marehemu wakati wakiwa hai Sinza Palestina, na baada ya zoezi hilo alipewa amri na mkubwa wake aendeshe gari la marehemu hao ambapo alipanda gari hilo na aliyekuwa mshitakiwa sita, Moris Nyangerela ambaye aliachiliwa huru na kulipeleka gari hilo kituo cha Urafiki.

Aidha walidai haya Gwasabi wakati akijitetea alikubali kushiriki kukamata na kuwapekua marehemu lakini aliamuriwa na mkuu wake apelike gari hilo Urafiki na mshitakiwa huyo alimleta shahidi wake, Nyangerela ambaye alikuja kudhibitisha hayo.

Hivyo wakaiomba mahakama hiyo itumie kifungu kile kile ilichokitumia kumwachia Nyangerela pia kitumike kumwachia Gwasabi na hivyo maoni na mapendekezo yao kwa mshitakiwa huyo wanaomba mahakama imwone hana hatia.

Wazee hao wakitoa maoni na mapendekezo yao dhidi ya mshitakiwa wa pili,SP-Christopher Bageni, wote kwa kauli moja wanakubaliana na upande wa mashitaka kwamba umeweza kudhibitisha kesi dhidi ya mshitakiwa na wakaiomba mahakama imuone ana hatia ya makosa anayoshitakiwa kwakuwa, ushahidi wa mazingira unaoyesha alitenda kosa hilo.

Kuhusu mshitakiwa tatu,SP- Ahmed Makelle, wazee hao kwa kauli moja waliomba mahakama imwone ana hatia kwasababu mashahidi wa upande wa mashitaka walimtambua mshitakiwa huyo alifika eneo la tukio na wakati mshitakiwa akijitetea alikiri kufika eneo la tukio na kwamba mashahidi hao walieleza walimtambua baada ya Makelle kuwa anagombea fuko la fedha.

Aidha wakitoa maoni yao kuhusu mshitakiwa wa tano, Jane Andrew,wazee hao pia waliomba atiwe hatiani kwani wanakubaliana na mashahidi wa upande wa mashitaka kwamba walimtambua kuwa ndiye aliyefika Sinza Palestina na alikuwa akigombea mfuko wa fedha.

Lakini katika hali isiyo tarajiwa na wengi, wakati wazee hao wa baraza walipomaliza kutoa maoni yao dhidi ya Mabula, Bageni, Makelle na Jane walikuwa wakiangua vicheko kizimbani.

Kuhusu mshitakiwa wa saba,Emmanuel Mabula, wazee hao pia walikubaliana na upande wa mshitaka kuwa umeweza kudhibitisha kesi kwa mshitakiwa huyo, kwani hakuna hata shahidi aliweza kuiambia mahakama siku ya tukio mshitakiwa huyo alipangiwa doria eneo la Makongo Juu.

“Mshitakiwa mwenyewe(Mabula) aliambia mahakama kuwa alikuwa ni miongoni mwa askari walioenda kupewa mkono wa pongenzi wa RCO-Zombe, huku akijua kuwa hakuwa hakuwa katika mapambano na majambazi lakini akakubali pongezi hizo, sisi tunasema aliku na lake jambo alilokuwa akilificha hivyo tunaomba hatiwe hatiani” alidai.

Wazee hao ambao walionyesha kujiamini wakati wakitoa mapendekezo yao, wakitoa maoni yao dhidi ya mshitakiwa tisa, Michael Shonza, walisema maoni yao kwa mshitakiwa hayo yanafanana na maoni waliyoyatoa kwa mshitakiwa saba, kwani siku ya tukio Mabula na Shonza walikuwa pamoja, hivyo wanameomba naye atiwe hatiani.

Aidha kuhusu mshitakiwa kumi, Koplo Abeneth Salo, wazee hao walisema baadhi ya mashahidi wa mashitaka walimtambua japo kuwa Januari 16/1/2006 Sinza Palestina alivalia nguo za kiraia na siku hiyo walimuona akiwa amekaa kwenye gari la mshitakiwa tatu(Makelle) ila mashahidi hao walimwona Jane na Makelle pale Sinza Palestina ila Abeneth alkuwa ndani ya gari.

Walikumbusha kuwa mshitakiwa 12(Rajabu) alieleza mshitakiwa tano(Jane) na Abeneth wote walifika barabara ya Samunujoma kwenye roli la Bidco, vile vile alimshuhudia Jane na Abeneth wakiondoka pamoja na gari la Makelle, na aliendelea kufahamisha mahakama kuwa gari hilo ndiyo lilikuwa la kwanza kuondoka .

Walisema Abeneth alipopewa haki ya kujitetea alidai yeye alishushwa Ubungo Terminal kwaajili ya kuendelea na doria na wala hakuweza kuleta shahidi ili adhibitishe madai hayo, hivyo walidai kushindwa kwa mshitakiwa huyo kufanya hivyo wanakubaliana na upande wa mashitaka kwamba wameweza kuthibitisha kesi dhidi yake na wakaiomba mahakama imwone ana hatia.

Aidha wazee hao wakichambua ushahidi wa mshitakiwa wa 12,Rajabu Bakari, walisema kwa hiari yake mwenye bila kulazimishwa na mtu yoyote ,mshitakiwa huyo akiwa ana akili timamu alikiri kuwa alikuwepo eneo la mauji msitu wa Pande na kwamba alipopewa haki ya kujitetea,mshitakiwa huyo alidai alikuwa chini ya amri ndiyo maana alikwenda katika msitu huo.

“Jaji huyu ni askari polisi na moja ya kazi ya majukumu yake ni kulinda usalama wa raia na mali zake,hivi kweli bosi wake anampa amri ya kuwa watu wasiyo na hatia, akanyamaza kimya?Mtukufu jaji huyu mshitakiwa anahusika moja kwa moja na tukio hili la mauji na tunaomba atiwe hatiani”alidai Magreth Mossi.

Baada ya wazee hao kuitimisha kutoa maoni na mapendekezo yao , Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, huo ndiyo mwisho wa kesi hiyo na kwamba hukumu ataitoa kutokana tarehe itakayopangwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Zombe na wenzake, wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Juni 27 ,2009
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 8:07 PM | Permalink | Maoni 0
Thursday, June 25, 2009
SERIKALI YASISITIZA ZOMBE ANA HATIA
Na Happiness Katabazi

UPANDE wa serikali katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane, umejigamba kuwa umethibitisha kesi hiyo pasipo shaka, hivyo kuiomba mahakama kuwatia hatiani washitakiwa hao kwa makosa waliyoshitakiwa.


Akiwasilisha majumuisho ya kesi hiyo jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Wakili wa Serikali, Mugaya Mtaki aliyekuwa akisaidiana na Angaza Mwipopo, Alexander Msikila na Justus Kaishozi, alidai katika kuthibitisha kesi hiyo, walileta mashahidi 37 na kutoa vielelezo 23.

Akichambua ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, Mtaki, alidai ushahidi uliotolewa na daktari umethibitisha kuwa marehemu hao walikuwa wamepigwa risasi na kuitaka mahakama kuondokana na dhana kwamba walipambana na polisi.

“Wakili wa utetezi, Majura Magafu, alitoa hoja ya kuwa hakukuwa na ubishi marehemu wote walikamatwa wakiwa hai. Sisi tunakubaliana na ukweli huo kwani umethibitishwa na shahidi wa 2, 6 na 7 wa upande wa mashitaka.

“Jambo jingine ambalo tunaomba mahakama yako ikubaliane na sisi kuwa halina ubishi, ni washitakiwa Zombe, Christopher Makele na Hemed Makele walikwenda Kituo cha Polisi Urafiki kushughulikia kielelezo cha fedha,” wakili wa serikali alimweleza Jaji Salum Massati.

Pamoja na hayo, wakili huyo aliiomba mahakama kuzingatia ushahidi wa mshitakiwa Makale uliodai Zombe ni muongo kwa kusema kuwa alikuwa hajui kilichokuwa kikitendeka, na kwamba yeye (Makele) aliandika taarifa za uongo kwa Tume ya Jaji Mussa Kipenka na ACP-Mgawe kwa maelekezo yake.

“Kwa muhtasari ushahidi huo ndiyo unamuhusisha Zombe kwa sababu alikuwa anajua tukio japo hakuwepo msitu wa Pande. Ni rai yetu Zombe aonekane na hatia kama washitakiwa wengine.

“Na hatua ya Msemwa (Wakili wa Zombe) kumfananisha Zombe na Yesu, kwamba anasulubiwa bila hatia, sisi tunasema mshitakiwa huyo hastahili kufananishwa na Yesu, kwani katika kesi ya Yesu, yule jaji wa Kirumi alikuwa na roho ya kikatili, ndiyo maana hakamtia Yesu hatiani licha ya Pilato aliuliza kuna ushahidi gani wa Yesu kutiwa hatiani.

“Katika kesi hii upande wa mashitaka tumethibitisha kesi yetu na wewe ni jaji unayesimamia haki, hivyo usifananishwe na jaji aliyemsulubu Yesu,” alidai Mtaki na kusababisha watu kuangua kicheko mahakamani.

Aliendelea kueleza kuwa, ushahidi wa utetezi unaonyesha kuwa Zombe hakuwapo msitu wa Pande, lakini alihoji ni kwa nini upande huo unashindwa kueleza wakati huo Zombe alikuwa wapi.

“Mtukufu Jaji, common intention siyo lazima washitakiwa wakae pamoja kupanga kabla ya kutenda kosa, kwa hiyo mahakama hii iuzingatie ushahidi uliotolewa kuwa washtakiwa wana hatia.

“Endapo Zombe na Gwasabi hawataonekana na hatia katika kesi ya mauaji, basi tunaomba washitakiwa hawa waonekane na hatia kwamba walishiriki kuficha kosa wakati likitendeka,” alieleza.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Salum Massati, aliwaasa wazee wa baraza, Magreth Mossi na Nicolas Kimolo, kutoa maoni yao kuhusu kesi hiyo kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

Pia aliwataka kutozingatia yale yaliyoripotiwa na vyombo vya habari, kwani yameandikwa mengi kuhusu kesi hiyo. Leo wazee hao wa baraza wanatarajiwa kutoa maoni yao ya mwisho katika kesi hiyo.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Zombe na wenzake, wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Juni 26,2009
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 7:38 PM | Permalink | Maoni 0
Tuesday, June 23, 2009
TUHARAKISHE KUTENGANISHA BIASHARA NA SIASA
Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni kundi la wananchi wa Kijiji cha Sing’isi, wilayani Arumeru walivamia shamba la Mbunge wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, Aloyce Kimaro (CCM), na kuchoma moto nyumba 20 na mazao mbalimbali yaliyokuwamo.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, uharibifu huo mpaka hivi sasa unakadiriwa kusababisha hasara ya kiasi cha sh milioni 500.

Kamanda Matei ameahidi kuwa uchunguzi wa kujua thamani halisi ya mali zilizoteketea unaendelea na kuna uwezekano wa hasara kuongezeka.

Wakati uchunguzi huo ukiendelea tayari watu 86 wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo na 38 wameshafikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka.

Naamini kuwa matukio ya namna hiyo yanayozidi kushamiri siku hadi siku ni matokeo ya mfumo wa kisiasa ulioparaganyika kiitikadi na kimaadili hapa nchini.

Kujinasibu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani na nje ya nchi kuwa ni watetezi wa wanyonge, wakati hawatendi hicho wanachokisema, ni moja ya mambo yanayowafanya watu wachoshwe na kuamua kufanya mambo ambayo ni kinyume cha sheria.

Kuwapo kwa sera nzuri na mipango ya serikali isiyo na utekelezaji pamoja na viongozi kuhubiri kile wasichokitenda, hubomoa daraja la mawasiliano baina yao na wananchi.

Wananchi huona viongozi wao kama wasaliti na wanyonyaji wa rasilimali zao kwa kujilimbikizia mali nyingi ilhali maisha ya wananchi yakizidi kuwa magumu kadiri siku zinavyosonga mbele.

Tujiulize, viongozi wa kujilimbikizia mali wameingia kwa utashi wa kuwahudumia wananchi au wajinufaishe kibiashara kupitia mwamvuli wa siasa?

Kuchanganya biashara na siasa ni mtego unaotakiwa kuteguliwa kwa uangalifu zaidi, kwa kuwa hata ikulu hivi sasa imekuwa ikitumika kwa manufaa ya viongozi, fulani wasiozingatia maadili ya viongozi wa umma.

Tunaweza kuendelea kama viongozi wataweza kujiepusha na mgongano wa kimasilahi kama ambavyo tunaona kila kukicha.

Inawezekana vipi rais mfanyabiashara akubali muswada wa kuibana biashara anayoifanya yeye au familia yake?

Tukifanikiwa kutofautisha na kutenganisha biashara na siasa tutaweza kuwadhibiti viongozi mbalimbali, kuanzia ngazi za chini mpaka juu kujihusisha na biashara na hapo tunaweza kurejesha angalau maadili ya viongozi wa umma.

Nimefarijika baada ya kumsikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani sheria hiyo itakuwa imeshaanza kufanya kazi.

Mifumo ya kiutendaji ndiyo inayowafanya wananchi kujiona ni wakimbizi katika ardhi yao, hatuna sababu za kuzidisha pengo kati ya walionacho na wasionacho ambalo mwisho wa siku ni vurugu miongoni mwa jamii.

Wananchi wanapenda viongozi wao washiriki katika shughuli za kilimo au nyingine za uzalishaji mali, lakini wasingependa kuona viongozi hao wanatumia madaraka yao kujineemesha.

Tusingependa nchi ikumbane na matatizo ya ardhi kama yale tunayoyaona Zimbabwe, Sudan na kwingineko.

Sina haja kuuhisha uvamizi wa Kimaro na itikadi za kisiasa, lakini ni vizuri dola ikaendesha jambo hilo bila kuingiza utashi wa kisiasa ili haki ipatikane.

Kimaro na kiongozi mwingine yeyote kwa hivi sasa hawazuiwi kufanya biashara, hivyo ni vema kwa wakati huu wakapatiwa ulinzi wa kisheria.

Mwisho, nimalizie kwa kuitaka serikali iliyo madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi iachane na utawala wa kiimla na mfumo wa kuwindana kama ule wa paka na panya.

Kama wataendelea na utaratibu huu, basi mbele ya safari hali itakuwa mbaya zaidi na tutabaini yupi ni panya na yupi ni paka.


Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Juni 21, 2009
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 3:56 PM | Permalink | Maoni 0
Tuesday, June 16, 2009
MAPAPARAZI WA MAHAKAMA:ACP-KENYELA KARIBU TENA KORTI YA KISUTU

Kushoto, Happiness Katabazi Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima na (kulia) ni mwandishi wa Gazeti la Uhuru, Furaha Omar, tukiwa tumepiga picha ya kumbukumbu na ACP-Charles Kenyela, jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, iki ni sekunde chache baada ya (njagu) huyo kufika katika mahakama hiyo kwa shughuli za kikazi alilakiwa kwa furaha na waandishi wa habari za Mahakamani.
Awali Kenyela ndiye alikuwa Mkuu wa Waendesha Mashitaka Kanda ya Dar es Salaam lakini hivi sasa ameamishiwa Makao Makuu ya Polisi Kanda Polisi jijini, kama Mkuu Kitengo cha Fedha.(Picha imepigwa Juni 16,2009)
 
© Happiness Katabazi |Tarehe: 2:11 PM | Permalink | Maoni 1